SABABU ZA MATAJIRI KURUDIA NGUO ZILE ZILE.
Kila siku tunafanya maamuzi mengi: unawaza niamke kutoka kitandani ama niendelee kulala kidogo, Ni muda gani niende kazini ama shuleni?, Leo nifanye mazoezi? na kama ndivyo, ni muda gani?, Nitakula chakula gani jioni? niendelee kufanya kazi au niende nyumbani? na mengineyo mengi
Kuna vitu vingi sana tunavyopaswa kuviamua kila siku. Maamuzi mengine huwa ni ya manufaa, lakini mengi huwa ni yenye manufaa kidogo au yasiyo na manufaa kabisa. Kwa bahati mbaya, tafiti zimeonyesha kuwa sisi kama binadamu, uwezo wetu wa kufanya maamuzi yaliyo sahihi na yenye manufaa una ukomo.
Hii inamaana kuwa kile unachokiamua mapema asubuhi, huwa na nguvu kuliko kile unachokiamua baada ya ubongo wako kuwa umeshachoka. Hali hii hujulikana kama maamuzi kulingana na uchovu, ni hali ya kisaikolojia ambayo hupelekea ufanywaji wa maamuzi kwa muda uliopo kupunguza ufanyaji wa maamuzi kwa wakati ujao.
John Tierney, mwandishi wa kitabu cha Willpower’ kilichouzwa sana na ‘The New York Times’ anasema,
“Kufanya uamuzi ukiwa na uchovu husaidia kueleza kwa nini kwa kawaida watu wenye busara hupata hasira wanapoongea na wenzao au na familia, wanatumia fedha nyingi kununulia nguo na kununua vyakula vingi wasivyoweza kuvimaliza kwa wakati. Haijalishi unavyojivuna kuwa na mantiki, huwezi kufanya maamuzi bila kupata madhara ya kibayolojia. Ni tofauti na uchovu wa kawaida wa kimwili. Huwezi kuwa makini kwa kiwango cha kujua kama umechoka, lakini nishati ya akili inakuwa katika kiwango cha chini kabisa.”
Maamuzi yote unayoyafanya yanatumia nguvu ya akili yako. Kitendo cha kufikiria tu ni ipi ya kuchagua kati ya A ama B kitakuchosha na kitapunguza nguvu yako ya ubongo. hii ina maana kuwa unavyofanya maamuzi mengi zaidi kwa siku, ndivyo uwezo wako wa kuamua unavyozidi kupungua.
Hii ndiyo sababu watu wengi wenye mafanikio makubwa kama Barack Obama, Steve Jobs, Mark Zuckerberg na Albert Einstein hupunguza kiwango cha maamuzi wanayofanya kwa siku nzima kwa kufanya vitu kama vile kurudia nguo.
Wanaelewa kuwa kupunguza muda wa kufikiri huwaongezea nguvu ya ubongo na muda wa kufanya mambo mengine.
Muda mwingi ambao Obama anautumia ofisini, huwa anavaa suti ya rangi ya kijivu ama ya bluu. Katika makala iliyoandikwa na Michael Leis iitwayo ‘Vanity fair’, Rais Obama alieleza kuwa ni kwa nini huwa anafanya hivyo,
“Utaniona nikiwa nimevaa suti ya rangi ya bluu ama ya kijivu. Ninajaribu kupunguza muda wa kufanya maamuzi. Sitaki kufanya maamuzi kuhusu kile nitakachovaa ama kula. Kwa sababu nina mambo mengi sana ya kuyafanyia maamuzi. Inabidi kuzingatia nguvu ya kufanya maamuzi yako. Inabidi ujizoeshe. Huwezi kuendesha shughuli zako za siku kama unasumbuliwa na mambo madogo madogo.”
Steve Jobs amejulikana sana kwa uvaaji wake wa fulana nyeusi, suruali ya jinsi ya bluu na raba za ‘New balance’ kila siku. Hii ilikuwa kama utambulisho wa muonekano wake na kama sehemu ya chapa ya ‘Apple’. Steve alijua kuwa ana ukomo wa kiwango cha nguvu ya ubongo katika kufanya maamuzi yenye tija. Kwahivyo kwake kuwaza nguo ya kuvaa kwa siku hiyo, ni sawa na kupunguza nguvu ya ubongo katika kuwaza kuhusu kampuni yake.
Albert Einstein alijulikana pia kwa kumiliki suti nyingi za rangi ya kijivu ili tu asipoteze muda mwingi katika kuamua atavaa nguo ipi kila asubuhi.
Kama huwa unapata shida ya kuamua vitu vidogo vidogo kila siku kama vile nguo gani ya kuvaa, utakua unaichosha akili yako kadri siku zinavyosonga. Ili kuokoa nguvu ya akili katika kuamua mambo ya msingi ya siku, inabidi ujifunze kubadilisha maamuzi yako ya kila siku ili uondokane na kuamua mambo yasiyo ya msingi yanayopunguza nguvu ya ubongo ya kufikiri.
Haya ni baadhi ya mambo unayoweza kuyafanya:
1.Kama Steve, Zuckerberg na Einstein, tafuta fulana chache, sweta, suruali na uzivae kama ambae umenunua nguo nyingi. Kimsingi, vaa nguo zilezile kila siku.
2. Panga muda maalumu wa kufanya mazoezi kila siku. usitumie nguvu nyingi ya ubongo kufikiria ni muda gani mzuri wa kufanya mazoezi.
3. Nunua mahitaji yako kwa muda uleule kila wiki.
4. Panga ratiba yako ya asubuhi. Asubuhi huwa imesongwa na maamuzi yasiyo ya msingi ambayo unaweza kujifunza kuyapanga, mfano nguo gani ya kuvaa, kula nini, muda wa kuondoka, muda wa kuamka na mengineyo mengi. Unaweza kuipanga maamuzi yako ya asubuhi yako kwa kubuni ratiba nzuri.
5. Panga vyakula vichache vya kula kila siku. hii itakusaidia kupata mlo bora, lakini lengo kuu hapa ni kwamba hutakuwa unawaza utakula nini, ama utapika mboga gani kila siku.
Haya ni mambo matano kati ya mengi unayoweza kuyafanya ili kupunguza kiwango cha maamuzi yasiyo ya msingi. Ki ukweli ni kuwa kwa kufanya hivi unaweza kupunguza ama kuondoa asilimia 80 ya maamuzi yasiyo ya msingi unayoyaamua kila siku. Unatakiwa kuielewa dhana hii na kujifunza kupunguza kufanya maamuzi yasiyo ya msingi sana.
Comments
Post a Comment